DSE Price Updates

                              TOL 330.00     TBL 1,800.00     TTP 510.00     TCC 1,640.00     SIMBA 1,780.00     SWISSPORT 650.00     TWIGA 1,340.00 -20.00     NICOL 305.00     DCB 360.00     KA 1,500.00     EABL 2,000.00     JHL 5,860.00    
LAST UPDATE: 24/9/2008 - 5:58PM EAT

Wednesday, November 5, 2008

Watuhumiwa wa EPA kizimbani leo

HABARI TOKA MICHUZI BLOG
watuhumiwa wa EPA kizimbani leo
JEETU Patel (pichani katikati) anayetajwa kuwa kinara wa ufisadi katika wizi wa Sh bilioni 133 kwenye Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) pamoja na wenzake tisa, jana walifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuiibia benki hiyo.
Wengine waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ni Devendra Vinodbhai Patel na Amit Nandy, Ketan Chohan, Johnson Lukaza, Bahati Mahenge, Davies Kamungu, Godfrey Mosha na Manase Mwakale anayeshitakiwa na mkewe, Eddah Mwakale, ambaye ndiye mwanamke pekee katika kesi hiyo ya kifisadi.
Jeetu, ambaye jina lake halisi ni Jayantkumar Chandubahi Patel, katika moja ya kesi anazokabiliwa nazo, anashitakiwa kwa pamoja na Devendra Vinodbhai Patel na Amit Nandy.
Kwenye shitaka hilo, washitakiwa wanatuhumiwa kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kuiba na kujipatia Sh bilioni 2.6 kwa kutumia kampuni yao ya Bencon ya Dar es Salaam. Wanadaiwa waliiba fedha hizo baada ya kudanganya kuwa Kampuni ya Matsushita Electric Trading Company iliwapa jukumu la kulipwa fedha hizo kupitia kampuni yao ya Bencon International Ltd.
Washitakiwa hao pia kwa pamoja wanashitakiwa kula njama, kughushi, kuiba na kujipatia tena Sh bilioni 7.9 kwa kutumia kampuni hiyo ya Bencon International Ltd. Katika wizi huo, washitakiwa hao wanadaiwa kudanganya kuwa walipewa jukumu la kulipwa fedha hizo na Kampuni ya Maruben Corporation ya Japan wakati wanajua kuwa si kweli.
Hakimu Euphamia Mingi alisema dhamana kwa washitakiwa ziko wazi, ila kila mshitakiwa anatakiwa kuweka mahakamani nusu ya fedha anazodaiwa kuiba, wadhamini wawili na mmoja kati yao awe ndugu wa karibu na wote watasaini hati ya dhamana.

Washitakiwa hao pia wanatakiwa kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani, wanatakiwa wasisafiri nje ya mkoa hadi kwa ruhusa ya mahakama. Sharti jingine ni kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi wataripoti kwa mwendesha mashitaka na pale wanapokuwa na matatizo, wadhamini wao watalazimika kwenda kutoa taarifa mahakamani.
Jeetu pia anashitakiwa katika kesi nyingine na Ketan Chohan na Amit Nandy ambao wanadaiwa kuiba Sh bilioni 3.3 kwa kutumia Kampuni ya Navy Cut Tobacco Tanzania Limited. Walidanganya kuwa wameruhusiwa na Kampuni ya Matsushita Electric Trading Company ya Japan walipwe fedha hizo. Kesi hiyo inasikilizwa na Hakimu Mkazi Neema Chusi na uamuzi wa dhamana yao utatolewa leo.
Kinara huyo wa ufisadi, pia anashitakiwa kwa wizi wa Sh bilioni 3.9 ambazo aliiba kwa kutumia kampuni ya Bina Rosorts Ltd kwa kudanganya kuwa walipewa mamlaka ya kulipwa fedha hizo na Kampuni ya C. Itoh & Company Ltd ya Japan. Katika shitaka hilo anashitakiwa kwa pamoja na wenzake Devenra Vinodbhai Patel na Nandy na kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Mkazi Richard Kabate. Katika shitaka jingine, Jeetu anashitakiwa kwa wizi wa Sh bilioni 4.9 kwa kushirikiana na Devenra na Nandy.
Wote wanatuhumiwa kufanya wizi huo kwa kutumia Kampuni ya Maltan Mining Company Ltd wakidanganya kuwa wameruhusiwa na Kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan walipwe fedha hizo na BoT.
Mtuhumiwa mwingine aliyefikishwa mahakamani jana ni Johnson Lukaza ambaye naye anatuhumiwa kula njama, kughushi, kuwasilisha hati ya uongo, kuiba na kujipatia Sh bilioni 6.3. Mtuhumiwa huyo na mwenzake aliyetajwa kwa jina la Mwesiga Lukaza ambaye hakuwapo mahakamani, wanadaiwa kufanya wizi huo Desemba 2005.
Dhamana kwa mshitakiwa iko wazi ila mshitakiwa anatakiwa kuweka mahakamani nusu ya fedha anazodaiwa kuiba na wadhamini wawili na mmoja kati yao awe ndugu wa karibu, wote watasaini hati ya dhamana. Mshitakiwa pia anatakiwa kuwasilisha hati yake ya kusafiria mahakamani, anatakiwa asisafiri nje ya mkoa hadi kwa ruhusa ya mahakama.
Sharti jingine ni kila Ijumaa ya mwisho wa mwezi ataripoti kwa mwendesha mashitaka na pale anapokuwa na matatizo wadhamini wao atalazimika kwenda kutoa taarifa mahakamani. Wengine waliopanda kizimbani ni Bahati Mahenge, Davies Kamungu, Godfrey Mosha na Manase Mwakale anayeshitakiwa na mkewe, Eddah ambaye ni mwanamke pekee katika kesi hiyo ya kifisadi.
Washitakiwa wanatuhumiwa kuiba Sh milioni 855.4 ambazo waliiba kwa kutumia Kampuni ya Changanyikeni Residential Complex Ltd baada ya kuwasilisha nyaraka za kughushi BoT wakionyesha kuwa kampuni hiyo, mkurugenzi wake Samson Mapunda ndiye aliyetoa idhini ya kulipwa fedha hizo.
Watu hao pia walishitakiwa kwa wizi wa Sh bilioni 1.2, mali ya BoT baada ya kutumia kampuni ya Changanyikeni Residential Complex Ltd wakidai wamepewa mamlaka ya kulipwa fedha hizo na kampuni ya Marubeni Corporation ya Japan. Uamuzi wa dhamana yao utatolewa kesho na Hakimu Victoria Nongwa.
Akihutubia Taifa Ijumaa iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alisema Sh bilioni 69.3 ambazo ni sawa na asilimia 76.7 ya Sh bilioni 90.3 zilizochotwa kutoka EPA, zilikuwa zimerejeshwa kufikia Oktoba 31. Hata hivyo, aliagiza kuwa wote ambao kufikia siku hiyo, watakuwa hawajatekeleza agizo la kurejesha fedha hizo, hatua za kisheria zichukuliwe.
Alitoa maelekezo kamili kwa ambao hawakutimiza malipo, majalada yao yakabidhiwe kwa Mkurugenzi wa Mashitaka mara moja, kwa hatua zipasazo za kisheria. Kampuni 23 zinadaiwa kuchota fedha, Sh bilioni 133 katika Akaunti ya Madeni ya Nje ya BoT, na iligundulika baada ya ukaguzi wa hesabu uliofanywa na Kampuni ya kigeni ya Ernst & Young katika mwaka 2005/2006 ambayo ilipewa kazi iliyoachwa na Deloitte & Touche ya Afrika Kusini.
kachelo koba kimanga 'assossa' (shoto) akimuelekeza jeethu patel pa kwenda wakati watuhumiwa wa EPA walipotinga mahakama ya kisutu sasa hivi kujibu tuhuma hizo
baadhi ya watuhumiwa wakiwa wamechuchumaa kusubiri kuingizwa mahakamani
baadhi ya watuhumiwa wa EPA wakisubiri kupanda kizimbani mchana huu katika mahakama ya hakimu mkazi wa kisutu, dar

Kwa habari kamili nenda:
http://www.habarileo.co.tz/kitaifa/?id=13538
na
http://dailynews.habarileo.co.tz/home/?id=8254

1 comment:

ROGERSBIZ said...

nice blog. road to riches. sijafwatilia hili swala kwa kirefu ila pesa walioiba ni nyingi sana.